HEKIMA (SWAHILI/KENYA)

SALA YA SOLOMONI YA KUMUOMBA MUNGU HEKIMA

INAOMBWA KUSOMA KILA SIKU NA WAKRISTU

IMETOLEWA KWA KITABU CHA HEKIMA 9:1-18

Omba hii sala mara nyingi kila siku. Ipatie watu wengi pia waombe Mungu wapate hekima. Sala zingine zapatikana kwa website hii: www.avemaria832.simplesite.com  Tangaza hii kwa watu wote ukitumia facebook etc.

  1. Ee Mungu wa babu, na Bwana wa rehema, ambaye ulivifanya vitu vyote kwa neno lako
  2. Na kwa Hekima wako ulimwumba mwanadamu apate kuvitawala viumbe vilivyofanywa nawe,
  3. Na kuuongoza ulimwengu kwa utakatifu na haki, na kutoa hukumu kwa unyofu wa moyo;
  4. Unipe Hekima, anayeketi karibu na kiti chako cha enzi, wala usinikatae miongoni mwa wana wako,
  5. Kwani mimi ni mtumishi wako na mwana wa mjakazi wako; mtu dhaifu, na muda mfupi wala sina nguvu za kuzielewa hukumu na sheria.
  6. Maana, hata kama mtu angekuwa mkamilifu kuliko wanadamu wote, mbali na Hekima atokaye kwako,  angehesabiwa si kitu.
  7. Wewe ulinichagua kuwa mfalme wa watu wako na mwamuzi wa wanao na bintizo.
  8. Uliniamuru kujenga hekalu katika mlima wako mtakatifu, na altare katika mji wa makao yako,    mfano wa hema takatifu uliyoitengeneza tayari tangu mwanzo.
  9. Na Hekima yu pamoja nawe, naye hujua matendo yako alikuwa karibu ulipofanya ulimwengu;   anafahamu ni nini kinachopendeza machoni pako, na nini ni sawa kadiri ya amri zako.
  10. Mpeleke kutoka mbingu takatifu, na kumtuma kutoka kiti chako cha enzi cha utukufu, Apate kutaabikia kazi pamoja nami, nami nijue ni nini kinachokupendeza.
  11. Maana Hekima hujua na kuelewa mambo yote, naye ataniongoza kuwa na kiasi katika kutenda kwangu, naye atanilinda katika utukufu wake;
  12.  Na hapo, matendo yangu yatakupendeza, nami nitawahukumu watu wako kwa haki, na kustahili kiti cha enzi cha baba yangu.
  13.  Maana nani kati ya wanadamu aweza kujua mashauri ya Mungu? Au kutafakari atakayo BWANA?
  14.  Kwani mawazo ya wenye kufa yana uoga, na fikra zetu zina hatari.
  15.  Maana mwili uharibikao huilemea roho na hema ya udongo hukandamiza akili yenye kujaa mawazo.
  16.  Ni vigumu kwetu kuyapambanua mambo ya duniani, na ni kazi ngumu kuyaona yaliyo mikononi mwetu; basi, yale yaliyo mbinguni nani atayachunguza?
  17.  Nani aliweza kuyajua mashauri yako,  isipokuwa wewe ulimpa Hekima, na kumpelekea roho yako takatifu kutoka juu?
  18.  Ndivyo yalivyonyoshwa mapito ya walio juu ya nchi nao wanadamu walifundishwa mambo yanayokupendeza, na wakaokolewa na Hekima.